Tatizo la kukatika kwa umeme kwenye mikoa ya Mtwara na Lindi, limewafanya mafundi wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) kukesha wakifanya ukarabati.
Imeelezwa kwamba mitambo minne kati ya tisa inayotumika kufua umeme kwenye Kituo cha Mtwara, imeharibika kwa wakati mmoja na kusababisha huduma kukatika kwenye maeneo mengi ya mikoa hiyo.
Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco, Kahitwa Bishaija aliyasema hayo mjini Mtwara juzi alipozungumza na baadhi ya wahariri wa vyombo vya habari waliotembelea kituo hicho.
Bashaija alisema mafundi walianza matengenezo ya mtambo mmoja, wakati kazi hiyo ikiendelea mingine mitatu ilizimika ghafla na kusababisha maeneo mengi kukosa huduma.
“Mitambo hii kila baada ya muda inahitaji kufanyiwa matengenezo,” alisema Bashaija.
Alisema ili kuhakikisha hali ya upatikanaji umeme kwenye mikoa hiyo inarudi kawaida, Tanesco imejipanga kuhakikisha tatizo linapatiwa ufumbuzi haraka.
“Lengo la Serikali ni kuona wananchi wanapatiwa umeme wa uhakika,” alisema Bashaija na kuongeza: “Tunatambua Waziri halali kutokana na tatizo hili kuwa kubwa, kwa hiyo mafundi hawa watafanya kazi usiku na mchana hadi hali itengemae.”
Naye Meneja wa Tanesco Kanda ya Kusini, Aziz Salum alisema Kituo cha Mtwara kinafua umeme wa laini 10 zinazolisha mikoa ya Mtwara na Lindi.
“Kituo hiki kinafua umeme kwa kutumia gesi asilia na kilianzishwa Machi 2007, kina uwezo wa kuzalisha megawati 18 na mpango wetu ni kuongeza megawati ili zifikie 22,” alisema Salum.
Alisema wanatarajia kujenga kituo kikubwa mkoani Mtwara kitakachozalisha umeme wa megawati 300, zitakazosaidia kuondoa tatizo la kukatika kwa nishati hiyo.
Akizungumzia tatizo la kukatika kwa umeme mkoani hapa, Salum alisema linachangiwa pia na ongezeko la matumizi kwa wateja.
“Kwetu tunaona ongezeko hili ni matokeo ya kukua kwa shughuli za uzalishaji, hivyo lazima sasa shirika na Serikali twende na kasi hii,” alisema.
Pia, alitoa wito kwa wananchi kuona umuhimu wa kulinda miundombinu ya umeme inayonunuliwa kwa gharama kubwa.
Salum alisema wanafanya jitihada ya kuongeza nguvu katika Kituo cha Kufua Umeme cha Mtwara Power Plant, ambacho kimefanyiwa usanifu wa kina ili kutoa huduma muda mrefu.
Akizungumzia hali ya huduma, Meneja wa Tanesco Mkoa wa Mtwara, Jafari Mpina alisema ili kuhakikisha wanasambaza umeme wa uhakika kwa wateja, licha ya kupunguza gharama za wataalamu wa nje ya nchi, wameunda Kikundi cha Kampuni Tanzu (Tidico).
Alisema kampuni hiyo kwa kiwango kikubwa imefanikisha ujenzi wa line za usafirishaji na usambazaji umeme zinazowezesha huduma hiyo kutoka Mtwara kwenda Lindi.
Meneja wa Kituo cha Kuzalisha Umeme kwa kutumia nishati ya gesi asili kwa mikoa ya Mtwara na Lindi, Mkurungwa Chinumba alisema kabla ya uwapo wa kituo hicho, mikoa hiyo ilikuwa ikitumia umeme unaozalishwa na mafuta ambao gharama zake ni kubwa.
Chinumba alisema kituo hicho kimesaidia kuongezeka kwa wateja na pato la Mtwara limekua.
“Kutokana na ongezeko la watumiaji wa umeme, jitihada zinaendelea kuhakikisha licha ya megawati 18 za sasa, Desemba tuongeze megawati 4 ili kuchochea uzalishaji,” alisema.
Mdororo wa uchumi
Mkazi wa Mtwara anayefanya kazi Hoteli ya Naf Beach, Michael Thomas alisema kukosekana kwa umeme wa uhakika kumesababisha mdororo wa uchumi.
Thomas alisema hali hiyo ambayo imedumu kwa takriban wiki mbili sasa imefanya hata hoteli yao kutetereka kwa mapato, kutokana na kutumia jenereta.
“Uzalishaji umekuwa mdogo huku gharama za uendeshaji zikipanda, tunatumia zaidi ya lita 300 za dizeli kwa usiku ambayo ni zaidi ya Sh600,000,” alisema Thomas ambaye ni mhasibu.
Pia, alisema ukosefu wa huduma hiyo umesababisha kununua maji kwa zaidi ya Sh400,000, hivyo kuiomba Serikali kuhakikisha inamaliza tatizo hilo haraka.
Mwishoni mwa wiki iliyopita Waziri wa Nishati, Dk Medard Kalemani alipokutana na watendaji wa wizara yake, wenyeviti wa bodi na watendaji wa Tanesco, Wakala wa Nishati Vijijini (Rea) na Kampuni ya Uendelezaji wa Jotoardhi Tanzania (TGDC), aliagiza Tanesco kuhakikisha tatizo la kukatika kwa umeme mkoani Mtwara linamalizika ili wananchi waendelee na shughuli zao za uchumi kama kawaida.
source:mwananchi.co.tz
0 comments:
Post a Comment