Kesi ya mauaji ya mfanyabiashara tajiri wa Mirerani, Erasto Msuya jana ilishindwa kusikilizwa baada ya mzee mshauri wa Mahakama Kuu kutokuwapo hivyo kusogezwa mbele hadi kesho.
Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Moshi, Benard Mpepo alisema mzee huyo ambaye hakumtaja jina alikuwa amesafiri kwenda nje ya mkoa kwa udhuru.
“Tulikuwa na wazee washauri watatu, lakini mmoja alifariki dunia kwa hiyo tukabaki na wawili. Kisheria hao wawili wangetosha kesi kuendelea lakini mmoja alisafiri hajarejea,” alisema.
Kutokana na tatizo hilo, Kesi hiyo inayovuta hisia za wananchi wengi hasa wa miji ya Mirerani wilayani Simanjiro Mkoa wa Manyara, Jiji la Arusha na miji ya Moshi na Bomang’ombe, sasa itaanza kusikilizwa kesho.Mfanyabiashara huyo aliyekuwa akimiliki vitega uchumi kadhaa, aliuawa kwa kufyatuliwa risasi 22 za bunduki aina ya SMG, huku 12 kati ya hizo zikimpata na kusababisha kifo chake. Tukio hilo lilitokea Agosti 7,2013 eneo la Mijohoroni wilayani Hai huku watu saba wakidaiwa kuhusika na mauaji hayo.
Kesi hiyo ilisimama kusikilizwa Machi 21 mwaka huu, baada ya upande wa mashtaka kuwasilisha notisi ya kukata rufaa kupinga uamuzi mdogo wa Jaji Salma Maghimbi anayesikiliza kesi hiyo.
Awali, kabla ya kusitishwa kwa usikilizaji wa kesi hiyo, kuliibuka mabishano ya kisheria kati ya mawakili wa utetezi na mawakili waandamizi wa Serikali wanaoendesha kesi hiyo. Mabishano hayo yalitokana na hatua ya shahidi wa tisa, Inspekta Samwel Maimu kutoa ushahidi wa mdomo wa kukiri kosa kwa mshtakiwa wa tatu, Ally Mussa bila kuwasilisha maelezo yake.
Mawakili wa utetezi, Hudson Ndusyepo, Majura Magafu, Emanuel Safari na John Lundu, walipinga utaratibu huo, wakisema ni kinyume cha sheria kwa vile maelezo hayo hayajapokewa mahakamani.
Jaji alikubaliana na hoja ya mawakili wa utetezi na kuzuia ushahidi huo, hali iliyochochea mawakili wa Serikali wakiongozwa na Abdalah Chavula kuwasilisha notisi ya kukata rufaa.
Kesi hiyo sasa imepangwa kuendelea kusikilizwa kwa siku 30 kuanzia kesho hadi Novemba 16 baada ya jopo la majaji wa Mahakama ya Rufaa lililoketi jijini Arusha kuitupa rufaa ya upande wa Jamhuri.
Washtakiwa katika kesi hiyo ni Sharifu Mohamed, Shaibu Jumanne au Mredii, Musa Mangu, Jalila Zuberi, Karim Kihundwa, Sadick Mohamed (Msudani au Mnubi) na Ally Mussa (Mjeshi).
source:mwananchi
0 comments:
Post a Comment