Ingekuwa mechi nzuri kwa Barcelona na ingeweza kuwa mbaya kwao pia. Mwishoni, sare ya 1-1 ugenini dhidi ya Atletico Madrid imekomesha rekodi ya ushindi wa asilimia 100 kwa miamba hao wa La Liga, lakini bado wameendelea kuwa mbele ya Real Madrid kwa tofauti ya alama tano Primera Division. Shukrani zote kwa Luis Suarez.
Suarez alikuwa na usiku mgumu katika mashambulizi kwa Barca, mara nyingi akiwa kushoto na Lionel Messi akiwa zaidi katikati, na kiwango chake cha sasa kimekuwa kikiwakera mashabiki kadhalika na mchezaji binafsi. Lakini pamoja na yote alifunga goli muhimu la kusawazisha.
Mchezaji huyo wa kimataifa wa Uruguay amechukua muda mrefu kuuguza majeraha msimu huu, na amefanya jitihada za ziada kurejea kwenye timu ya taifa lake kufuzu Kombe la Dunia na pia amecheza nafasi tofauti chini ya kocha mpya Ernesto Valverde.
Huenda akawa mchezaji anayelihisi zaidi pengo la Neymar aliyetimkia Paris Saint-Germain majira ya joto na majeraha ya Ousmane Dembele pia, ambayo yameivuruga uwiano mzuri wa safu ya mashambulizi ya Barca iliyopungukiwa nguvu dhidi ya Atletico Jumamosi.

"Inawezekana alifanya kazi kubwa [kurejea]," kocha wa straika huyo katika timu ya taifa ya Uruguay, Martin Lasarte, aliiambia Goal. "Ni mchezaji imara kifiziki na anapokuwa mzima kamili, ni kama fahali. Hayupo katika kiwango chake kwa sasa."
Na aliongeza: "Suarez hucheza zaidi kama winga. Hajafunga kwa kiwango chake akiwa nafasi hiyo. Lakini ni kwamba anazoea nafasi hiyo. Kwangu mimi, ni mshambuliaji wa kati, lakini wachezaji bora sana hujizoeza kucheza kokote na hilo ndilo analopaswa kufanya."
Suarez, kama ilivyo kwa Barca, aliimarika mechi hii ilivyokuwa ikiendelea. Na ukweli ni kwamba Barca walikuwa bora zaidi Valverde alipobadili mfumo kuwa 4-3-3, baada ya kuanza kwa mfumo wa 4-4-2 Andre Gomes akionekana kuwa chaguo baya sehemu ya kiungo.
Gomes ana mbinu nzuri na anapeleka mpira mbele nyakati zote, kadhalika akiwa ni mchezaji shupavu. Lakini bado haonekani kuwa mchezaji sahihi kwa Barcelona hadi sasa, huu ukiwa ni msimu wake wa pili kwa klabu hiyo ya Catalan.


Mreno huyo hana kasi na inaonekana anapunguza kasi ya mashambulizi kwa Barca. Mara nyingi ni rahisi kumsoma anachotaka kufanya na ufanisi wa timu huonekana kushuka kila anapopewa fursa ya kuanza kikosi cha kwanza. Ni vigumu kuona anachoisaidia timu katika kiwango hiki.
Mambo ni tofauti kwa Suarez. Ukitoa penalti, mchezaji huyo wa kimataifa wa Uruguay amefunga magoli 85 La Liga tangu 2014-15, zaidi ya mchezaji mwingine yeyote isipokuwa Lionel Messi (102) na Cristiano Ronaldo (87). Na Jumamosi, goli lake la kichwa lilifuta bao matata la Sauli ambalo lilitaka kuizamisha Barca shimoni.
"Ni mchezaji anayeweza kupotea dimbani kwa muda," kocha wake wa timu ya taifa Oscar Tabarez alisema. "Mara nyingi kwenye mechi za kufuzu tulifikiria kumwondoa lakini ghafla aliimarika na kufunga magoli. Ni mchezaji ambaye huwezi kumwainisha kwa kiwango chake."



0 comments:
Post a Comment