Kingunge ametoa kauli hii leo nyumbani kwake jijini Dar es Salaam mbele ya waandishi wa habari wakati akiongelea mvutano kati ya Chadema na serikali unaoendelea kwa sasa.
Chadema kimeingia kwenye mvutano
mkubwa na serikali kutokana na dhamira yake ya kufanya mikutano na
maandamano nchi nzima chini ya mwavuli wa Umoja wa Kupinga Udikteta
(Ukuta).
Hivi karibuni, Rais John Magufuli
alisisitiza kutoruhusu maandamano na mikutano ya kisiasa na kuagiza
kuwa, wanaotaka kufanya mikutano wafanye ndani ya mipaka ya majimbo yao
na si vinginevyo jambo ambalo Chadema wanapinga.
Hali hiyo imeibua mtikisiko mkubwa
nchini huku kada mbalimbali ikiwa ni pamoja na viongozi wa dini,
wanasiasa, wasomi na wananchi wa kawaida wakitaka kupatikana suluhu
kabla ya Septemba Mosi, tarehe iliyopangwa kuanza maandamano na mikutano
hiyo.
Kwenye mkutano wake na wanahabari
Kingunge anawalaumu viongozi wastaafu wakiwemo marais pamoja na mawaziri
wakuu kwa kukaa kimya wakati huu ambao nchi inatikishwa huku Katiba ya
Jamhuri ikisiginwa.
Miongoni mwa viongozi wanaolalamikiwa
kutosikika ama kuchukua hatua zozote ili kuilinda Katiba ni pamoja na
Marais Wastaafu, Alhaj Ali Hassan Mwinyi, Benjamin Mkapa na Aman Abeid
Karume (Zanzibar).
Viongozi wengine waliotajwa ni Mawaziri Wakuu Wastaafu, Cleopa Msuya; Jaji Mstaafu, Joseph Warioba.
“Mzee Mwinyi yupo kimya, Mkapa kimya, Warioba kimya, Cleopa Msuya kimya, Amani Karume kimya,” amesema Kingunge na kuongeza;
“Ukimya huu unatokana na nini? Hawa
wote waliwahi kula viapo vya utii kwa Katiba. Mimi nahoji, wazee
wenzangu vipi mnakuwa kimya? Nawaambia kuwa mnachofanya si sawa.
“Naomba wazee wote tujitokeze kuhesabiwa katika hili la uvunjifu wa Katiba na sheria.”
Kingunge ambaye alihamia Chadema
akitokea CCM kabla ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana kutokana na
kutoridhishwa na namna mchakato wa kumpata mgombea urais kutoka chama
hicho amesema, Chadema inatumia haki yake ya kikatiba.
“Naomba Rais Magufuli, akubali
kuitisha kikao na Chadema ambacho pia wazee wastaafu watahudhuria,
akifanya hivyo hata sisi wazee tutawageukia Chadema na kuwambia
wasitishe mpango wao wa maandamano,” amesema.
Amesema kwamba, kibaya zaidi Jeshi la
Polisi linaandaa bunduki kwa ajili ya kupambana na raia ambao hawana
kitu na kuwa, hali hiyo haipaswi kuvumiliwa.
Mwanasiasa huo amesema, Chadema
wameamua kutetea haki yao ya kikatiba na kisheria kwa kufanyaa
maandamano kote nchini, na kina wafuasi wengi hivyo si jambo la kubeza.
“Upande wa pili, lipo Jeshi la
Polisi na watawala ambao wanaahidi kuwakabili. Kwa bahati mbaya polisi
na watawala hawatetei Katiba wala Sheria,” amesema.
Amesema kuwa, Tanzania kwa sasa
inakabiliwa na ombwe la uongozi na kwamba, nchi imekosa watawala wenye
sifa thabiti ya kuongoza taifa.
“Kwa hakika, tatizo kubwa la sasa
la nchi yetu ni ombwe la kiuongozi, kwasababu kama ni watawala tunao
kweli kweli, lakini tunachokosa ni watawala wenye maarifa ya kiuongozi.
“Inashangaza kuona wazee wastaafu kukaa kimya wakati nchi inakabiliwa na tatizo linaloweza kutuangamiza.
“Upande mmoja unanoa mapanga,
unaanda bunduki kwa ajili ya kuchinja na kuua na upande wa pili wapo
raia tu, tena wasio na silaha zozote.”
Kingunge anasema, wananchi ambao serikali na Jeshi la Polisi wanajiandaa kupambana nao, wanalilia Katiba na sheria zifuatwe.
“Laiti kama Chadema wangekuwa
hawatetei Katiba na sheria, kungekuwa na kila sababu ya kuwashughulikia,
lakini kwa kuwa wanatetea Katiba na sheria, kuna umuhimu wa kuyapa
uzito madai yao,” amesema Kingunge.
Mwanasiasa huyo amesema kuwa, mvutano
wa sasa sio wa Chadema na serikali isipokuwa ni suala la wananchi wote
wa wenye mapenzi mema na taifa lao.
0 comments:
Post a Comment