Pages

Subscribe:

Thursday, 25 August 2016

Ujio wa Mourinho umeleta athari gani kwa Rashford na Chipukizi wa Manchester United?

Ujio wa Mourinho umeleta athari gani kwa Rashford na Chipukizi wa Manchester United?
Zlatan Ibrahimovic ni Mfalme wa Manchester United, anaongoza kwa swaga, Pogba naye ni mnyama hatari, Je! kuna nafasi kwa watoto?

Mourinho alipokuwa kwenye mchakato wa kutua United, hofu ilitanda kwa wachezaji chipukizi wangepata nafasi Old Trafford na hili linaonekana kuwa na adhari tayari
Wachezaji wa akademi ya Manchester United wameanza kujawa na hofu kutokana na tabia ya kocha Jose Mourinho kutokuwa na imani na wachezaji kinda. Ujio wa Zlatan Ibrahimovic na Pogba umeongeza nguvu kwenye kikosi cha United lakini ni dhahiri hakuna mchezaji kinda atakayepata namba mbele ya masupastaa hao.
Marcus Rashford ni miongoni mwa wachezaji walioathiriwa na utawala mpya wa Jose Mourinho pale Old Trafford.
Uamuzi wa Mourinho kutomjumuisha hata kwenye benchi Marcus Rashford katika michezo miwili mfululizo tayari umeanza kuwapa mashaka mashabiki na wachezaji wengine chipukizi.
Tayari amemuuza mchezaji Tyler Blackett kwenda Reading na kumtoa kwa mkopo Cameron Borthwick-Jackson kwenda Wolves, uamuzi ambao umeanza kuwapa United mashaka juu ya mustakabali wa vijana kwenye timu yao.
Kipigo cha timu ya vijana chini ya miaka 23 dhidi ya vijana wenzao wa Southampton kwenye dimba la St Marys kimeleta mshtuko mkubwa, huku wengi wakiuliza ni kwanini wachezaji kama Andreas Pereira, Memphis Depay, Rashford na Will Keane hawakuchezeshwa.
Wachezaji ambao walikuwa wakipata nafasi kwenye kikosi cha wakubwa sasa wanakosa namba kwenye kikosi cha vijana wadogo.
Kwa Rashford kukosa nafasi ya kucheza kumeanza kumletea athari, ambapo meneja wa timu ya taifa ya Uingereza Sam Allardyce amekiri kwamba haoni sababu ya kumjumuisha kwenye kikosi chake licha ya kuonesha kiwango bora msimu uliopita na kwenye Michuano ya Euro mwaka huu.
“Kwa sasa Rashford hapati muda wa kucheza, hivyo itaniwia vigumu sana kumjumuisha kwenye kikosi changu, maana siwezi kumfikiria kwa kiwango cha msimu uliopita ilhali kwa sasa hachezi,” alisema Allardyce.
Kuondoka kwa mkopo kwa wachezaji Blackett na Borthwick-Jackson, Guillermo Varela, Adnan Januzaj na James Wilson, huku Paddy McNair na Donald Love wakiondoka moja kwa moja, kunawaacha United wakiwa hawana tena vijana wanaoweza kucheza kikosi cha wakubwa ukiwaondoa Jesse Lingard na Rashford.
Kwa wachezaji waliobakishwa ambao ni Timothy Fosu-Mensah, Pereira, Keane, Joe Riley, Regan Poole na James Weir hawana nafasi ya kucheza kwenye kikosi cha wakubwa na hata hivyo pia wanaweza kutolewa kwa mkopo kabla ya dirisha la usajili kufungwa.

Hali hii inayotokea kwa sasa, si ngeni sana kwani hata Van Gaal alifanya hivyo msimu uliopita baada ya kuwatoa kwa mkopo Januzaj na Blackett pia, lakini aliamua kutoa nafasi ya kucheza japo kwa uchache kwa mchezaji Pereira na baadaye kumjumuisha Rashford na Lingard ambao walionesha uwezo mkubwa kwenye michezo waliyocheza.
Borthwick-Jackson ataongeza uwezo zaidi kwa kupata nafasi kubwa kwenye kikosi cha Wolves kuliko kukaa na kusubiri mpaka Luke Shaw aumie au kushuka kiwango. Pereira atakuwa na nafasi nzuri kwenye kikosi cha Fulham kuliko kubaki klabuni hapo na kusotea benchi.
“Mourinho ameniambia kwamba, ana malengo makubwa na mimi na anaona kuna dalilia nzuri kwa maisha yangu ya baadaye kwenye soka,” Borthwick-Jackson alisema wakati alipokamilisha utaratibu wa kujiunga na Wolves kwa mkopo.
“Hivyo kikubwa ninachokiangalia hapa ni kupata uzoefu ili niweze kupata nafasi katika kikosi cha United.”
Kwa wale ambao bado wamebakishwa na Mourinho wanatakiwa kuwa na imani na kocha wao, maana alishawaambia kwamba muda wao wa kucheza utaanza mwezi Septemba kwenye Kombe la Ligi na Europa.

Kwa upande wa Borthwick-Jackson, Januzaj na wengine wanapaswa kujituma na kumridhisha kocha wao ili aweze kuwaamini na kuwarejesha kikosini. Licha ya kuwaondoa moja kwa moja wachezaji McNair na Blackett, lakini naamini United hawatarudia makosa waliyofanya kwa Pogba.

Ujio wa Jose Mourinho utawarejeshea Manchester United hadhi yao, uwepo wa Mfalme Zlatan Ibrahimovic na Pogba umeanza kuleta tumaini jipya.

0 comments:

Post a Comment