Mvutano
kuhusu maelezo ya mlalamikaji katika kesi ya uchochezi inayomkabili
Mbunge wa Singida Mashariki Tundu Lissu, baina ya mawakili wa upande wa
mashtaka na upande wa utetezi ulikwamisha usikilizwaji wa kesi hiyo.
Katika kesi hiyo Lissu ambaye pia ni
Mnadhimu wa Kambi ya Upinzani Bungeni na Mwanasheria wa Chama cha
Demokrasia na Maendeleo (Chadema) anadaiwa kutoa kauli za uchochezi
dhidi ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano.
Anadaiwa kuwa Juni 28, mwaka huu,
Lissu akiwa katika viwanja vya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, alitoa
kauli za uchochezi kuwa:
“Mamlaka ya Serikali mbovu ni ya
kidiktekta uchwara inahitaji kupingwa na kila Mtanzania kwa nguvu zote,
huyu dikitekta uchwara lazima apingwe kila sehemu. Kama uongozi
utafanywa na utawala wa kijinga nchi inaingia ndani ya giza nene.’’
Kesi hiyo ilitarajiwa kuanza
kusikilizwa leo kwa upande wa mashtaka kuanza kutoa ushahidi.Wakili wa
Serikali Bernard Kongola aliieleza mahakama kuwa walikuwa na mashahidi
wawili ambao aliwataja kuwa ni Mrakibu Msaidizi wa Polisi (ASP) Kimweli
na Staff Sajenti Ndege.
Hata hivyo kabla ya kesi hiyo
kusikilizwa, kiongozi wa jopo la mawakili wa Lissu, Peter Kibatala
aliiomba mahakama wapewe maelezo ya mlalamikaji katika kesi hiyo kabla
ya kufanya jambo lolote, jambo ambalo liliibua mvutano wa hoja baada ya
kupingwa na upande wa mashtaka.
Wakili Kongola aliieleza mahakama kuwa
mlalamikaji katika kesi hiyo ambaye ni Kamanda wa Polisi wa Kanda
Maalum Dar es Salaam, si miongoni mwa mashahidi wao wanaokusudia kuwaita
mahakamani.
Pia alisema kuwa kwa mujibu wa sheria hawalazimiki kutoa maelezo hayo ya mlalamikaji kwa mtu ambaye si shahidi.
Akijibu hoja hizo, Wakili Kibatala
alidai kuwa taarifa ya huyo mlalamikaji ndio chanzo au iliyosababisha
kesi hiyo na kwamba iwapo watamleta au hawatamleta lakini maelezo yake
ni sehemu ya kesi hiyo.
Alidai kuwa hata mashtaka yaliyopo chini ya sheria ya magazeti ni ya muhimu na kwamba hawawezi kujitetea bila kuyaona na kwamba hata kama upande wa mashtaka hautamuita, wao wataiomba mahakama aitwe kwa lazima.
Hivyo aliiomba mahakama iulazimishe upande wa mashtaka uwapatie maelezo hayo ya mlalamikaji.
Baada ya kusikiliza hoja hizo, Hakimu
Dk Yohana Yongolo aliahirisha kesi hiyo hadi Septemba 6, mwaka huu,
atakapotoa uamuzi, baada ya kupitia vizuri hoja za kisheria za pande
zote.
0 comments:
Post a Comment